Huku akiandamwa na kesi juu ya kesi, Miss Tanzania 2006/07 anayewika kwenye tasnia ya filamu za Kibongo, Wema Abraham Sepetu (23), ameanguka ghafla na kuzimia kisha kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Kwa mujibu wa chanzo makini, tukio hilo lilijiri jijini Dar es Slaam Ijumaa iliyopita ambapo mnyange huyo alitakiwa kutimba katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, kwa ajili ya kesi inayomkabili ya kutoa lugha chafu na kumtishia maisha mshiriki wa Miss Kiswahili 2009, Rehema Fabian.
Ilidaiwa kwamba, akiwa njiani kuelekea kituoni hapo, Wema alianguka na kuzimia baada ya kupewa taarifa kuwa askari wa Kituo cha Magomeni, Dar walikuwa wamemuwekea mtego mahali hapo ili kumnasa kwa soo lingine jipya.
Ijumaa Wikienda ambalo lilikuwa limeweka kambi kituoni hapo, lilifanya kazi yake na kugundua kuwa, kulikuwa na mapaparazi kutoka chombo kimoja cha habari (Siyo Global) waliokuwa wakimsubiri Wema atimbe mahali hapo ili kupata picha za tukio lingine la kukamatwa.
Katika kuwadodosa mapaparazi hao, ilidaiwa kuwa, kuna jamaa mmoja jina halikupatikana aliyefungua kesi mpya akidai kutapeliwa simu na mrembo huyo.
TUKIO LA KUZIMIA
Akifunguka juu ya tukio la kuzimia, Wema aliyefunika ajabu kwenye Filamu ya The Diary alisema kuwa alipokea ujumbe mfupi ‘sms’ kwenye simu yake ya kiganjani kwamba, kuna kila dalili akakamatwa kwa ishu nyingine.
“Kusema kweli baada ya hapo sikujua kilichoendelea hadi nilipozinduka nikajikuta hospitalini,“alisema Wema.
UJUMBE WA KUJIUA WASAMBAA
Mara baada ya kurejea katika hali yake ya kawaida, Wema aliandika ujumbe wa kukata tamaa ya maisha katika ukurasa wake kwenye Mtandao wa Facebook ulioibua hofu kwamba huenda akajiua kutokana na matatizo yanamwandama.
Katika hilo, Ijumaa Wikienda lilimuuliza undani wa ujumbe huo ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Niliandika ujumbe wa kuyachoka maisha kwa sababu nilikuwa na hasira sana, nilihisi nasakamwa bila sababu yoyote.
“Nashukuru watu wengi waliniandikia meseji wakiniuliza kwa nataka kujiua, niliwaambia nilifikiria hivyo kwa sababu kila siku naona kama kuna kitu nimemkosea Mungu ‘so’ ni bora nipumzike.
“Nisaidieni kuwaambia mashabiki wangu wasinichukie, nawaahidi zawadi ya filamu yangu mpya ya The Diary itakayoingia mtaani mwezi huu.”
Kama Wema angetiwa tena mbaroni kwa soo la simu, ingekuwa ni mara ya nne kutimba polisi ndani ya kipindi kifupi cha ya miezi miwili.
taarifa toka global publishers...
No comments:
Post a Comment